emblem

ARDHI UNIVERSITY

News and Events

Kongamano la Wanawake Chuo Kikuu Ardhi

 

Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, Wafanyakazi wanawake wa Chuo Kikuu Ardhi leo tarehe 3.03.2023 wameandaa Kongamano lenye lengo la kukumbushana mambo mbalimbali yanayohusu ustawi wa wanawake katika kuboresha utendaji kazi Chuoni.

Kongamano hilo lilianza kwa Maandamano yaliyoanzia jengo la Utawala kuelekea Viwanja vya ARISA ambapo waandamanaji waliimba nyimbo mbalimbali zenye kuhamasisha Ari ya wanawake kwenye ufanyaji kazi na kuchukua majukumu muhimu kwenye ngazi ya familia, kazini na Taifa kwa ujumla.

Aidha Kongamano hilo lilifuatiwa na Semina ambapo Mgeni rasmi katika semina hiyo alikuwa ni Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Evaristo Liwa ambae aliwapongeza wanawake kwa kufanya kazi kwa umahiri iliyopolekea kuwa na idadi kubwa ya viongozi wanawake katika ngazi ya Menejimenti.

"Mmekuwa mkifanya kazi inayoonekana, sina shaka na utendaji wenu ambao umepelekea wengi wenu kuwa viongozi wa ngazi za juu hapa Chuoni." Alisema Prof. Liwa wakati wa ufunguzi wa Semina hiyo.

Nae Bi. Lydia Gunzu ambae ni Mratibu Mkuu kamati ya Wanawake tawi la ARU - THTU amesema, semina hiyo imeandaliwa ili kukumbushana mambo muhimu ambayo yatasaidia katika kuboresha utendaji kazi Chuoni.
Amesema mada zote zilizowasilishwa zimeendana na Kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni "Ubunifu wa mabadiliko ya teknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia"

Katika semina hiyo mtoa mada Bi. Julieth Mchunguzi kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii aliongelea kuhusu afya ya akili huku Bwn. Husama Nurdin wa Idara ya mafunzo ya Biashara kutoka  Chuo Kikuu Ardhi aliongelea kuhusu  usimamizi wa fedha binafsi na maandalizi kabla ya kustaafu.